Mbunge wa Daadab, Mhe. Farah Maalim, Afurushwa Kutoka Chama cha Wiper Democratic Movement
Ripoti ya Steve El Sabai
Maalim, ambaye pia ni miongoni mwa wanasiasa maarufu katika eneo la Kaskazini Mashariki, alikua na uhusiano wa karibu na chama cha Wiper chini ya uongozi wa Kalonzo Musyoka. Hata hivyo, kufukuzwa kwake kutoka chama kumechochewa na ukosefu wake wa nidhamu na kauli zake za hivi karibuni ambazo zimeelezwa kama kashfa kubwa.
Miongoni mwa matukio yaliyosababisha hatua hii ni kauli za Maalim kuhusu vijana na wanawake, akizungumza kwa namna isiyofaa kuhusu sehemu zao za siri. Kauli hizi zilichochea hasira kubwa kutoka kwa viongozi wa chama cha Wiper na kinara wake, Kalonzo Musyoka, ambaye alisisitiza kuwa kauli za Maalim hazikubaliki wala si za kiungwana katika siasa za chama hicho. Viongozi wa chama walielezea kutokubaliana na mtindo wa kisiasa wa Maalim, wakisema kuwa ni kinyume na misingi ya chama.
Maalim ameonyesha kutoridhika na uamuzi huu, akisema kuwa uamuzi wa chama hauwezi kubadili dhamira yake ya kuendelea kuwahudumia wananchi wa Daadab na kanda hiyo kwa ujumla. Aidha, amesisitiza kuwa ataendelea kutetea maslahi ya wapiga kura wake bila kujali uamuzi wa Wiper.
Wakati huu, maswali kuhusu hatma ya kisiasa ya Mhe. Maalim yanaendelea kushika kasi huku wafuasi wake wakituma salamu za mshikamano na kumtaka kuendelea na mapambano ya kisiasa kwa manufaa ya jamii yake.

Comments
Post a Comment